Wanaobambwa kwa rushwa CCM hawana chao | Send to a friend |
Saturday, 24 July 2010 10:00 |
0diggsdigg SIKU moja baada ya kuripotiwa matukio rushwa katika mchakato kupata wagombea ubunge ndani ya CCM, chama hicho kimesema mgombea yeyote atakayekamatwa na Takukuru hatapitishwa hata kama atashinda katika kura za maoni. Chama hicho kimepongeza mkakati wa Takukuru kuwanasa wagombea waojihusisha na rushwa na kusema chenyewe kinaandaa adhabu kali kwa watakaothibitika kuhusika na vitendo hivyo. Katibu Mkuu Yusuf Makamba aliliambia gazeti hili jana CCM itawafutia matokeo wagombea wote watakaothibitika kujihusisha na rushwa katika mchakato huo bila kujali majina na nyadhifa zao ndani ya chama. "Tunaomba wanachama watusaidie kwanza kwa kutowachagua watu wa aina hiyo. Lakini ikitokea bahati mbaya wamechaguliwa, hatutampitisha. Msimamo wetu CCM ni kutomtetea mgombea yoyote anayetoa rushwa," alisisitiza Makamba. Makamba aliipongeza Takukuru kwa kazi hiyo ya kupambana na rushwa na kuitaka isimwogope mtu badala yake iongeze kasi ya kuwafuatilia na kuwachukulia hatua. "Mimi sijapata taarifa rasmi kama kuna wagombea wamekamatwa na Takukuru kwa rushwa, lakini naipongeza kwa kazi hiyo nzuri, naipongeza, iongeze bidiina wanaCCM washirikiane na Takukuru kufichua watoa na wala rushwa," alisema Makamba. Kauli ya Makamba imekuja huku taarifa za rushwa zikiendelea kuripotiwa katika kampeni hizo za kura za maoni zilizoanza juzi nchini kote. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amewaonya wanasiasa kutojiingiza katika matendo ya rushwa kwa kuwa taasisi yake haitanii katika suala hilo. “Takukuru hatutanii, we mean business (tupo kazini) na hatufanyi danganya toto hapa.... Nawasihi wasitoe wala kupokea rushwa,” alisema Dk Hoseah. Alisema mpaka sasa Takukuru imeshakusanya taarifa mbalimbali za kiintelijensia kuhusu matukio ya rushwa na punde watuhumiwa wataanza kuhojiwa. “Tumeshakusanya taarifa za kiintelijensia za kutosha hivyo nawasihi wanasiasa pamoja na wananchi kwa ujumla tusilaumiane maana tumejipanga vizuri sana,” alisema Dk Hoseah. Mkoani Mwanza Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Mbunge wa Magu Dk Festus Limbu ameonja shubiri ya Takukuru baada ya kukamatwa akitoa Sh5000 kwa mpigakura. Tukio hilo lilitokea juzi jioni wilayani Magu wakati wagombea wa ubunge kupitia CCM walipokuwa wakijinadi na kuomba kuteuliwa katika kura za maoni. Habari zimeeleza kuwa Dk Limbu alikamatwa saa 10:00 jioni na kuhojiwa kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 5:00 usiku, huku wagombea wengine wakihojiwa kwa nyakati tofauti kuhusu tukio hilo ndani ya muda huo. Kamanda wa Takukuru mkoani Mwanza Christopher Mariba alithibisha tukio hilo na kueleza kuwa Dk Limbu alitoa fedha hiyo kwa mmoja wa wapiga kura, mbele ya wagombea wenzake wakati wakitoka katika mikutano ya kampeni. Mariba alilieleza gazeti hili jana kuwa Takukuru ilimshikilia Dk Limbu kwa muda pamoja na mtu aliyepokea fedha hiyo kwa ajili ya mahojiano. “Tukio hilo lipo, lakini kwa sasa tunaendelea na uchunguzi, siwezi kutoa maelezo zaidi,” alieleza kamanda huyo. Hata hivyo habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa baada ya kutoa fedha hizo, wagombea wenzake walimkamata aliyepokea na Dk Limbu na kuwapigia simu maofisa wa Takukuru ambao walifika na kumchukua. Lakini, Dk Limbu alipoulizwa na gazeti hili jana alikana kushikiliwa na Takukuru na kueleza kuwa kulitokea ni kutoelewana kidogo tu baina yake na wagombea wenzake. “Hiki ni kipindi cha kampeni, kila mtu anataka kuvutia kwake, jambo hili halipo. Kilichotokea ni kutoelewana tu basi na mtu mmoja akaamua kuwapigia simu Takukuru,” alieleza Dk Limbu kwa kifupi. Mkoa wa Lindi Takukuru mkoani Lindi imewakamata na kuwahoji wajumbe watatu wa kamati ya siasa ya wilaya ya Lindi kwa tuhuma za kugawa fedha kwa wanachama wa CCM ili kuwashawishi wamchague mgombea wanayemuunga. Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika wilaya ya Lindi mjini ambako wajumbe hao walikuwa wanagawa fedha hizo kwa wajumbe wa matawi ili kuimarisha ushawishi huo. Kamanda wa Takukuru wilaya ya Lindi, George Mbwiga zilisema kuwa Takukuru iliwakamata wajumbe hao baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanagawa fedha kwa wanachama wa CCM. "Tukio hilo, ni kweli. Tuliwaita na kuwahoji baada kupata taarifa kuwa waligawa fedha na baadaye tulimewaachia huru", alisema Mbwiga. Mkoa wa Mara Baadhi ya wanaCCM wanaoomba kuteuliwa na chama hicho kugombea ubunge katika majimbo ya mkoa wa Mara wamepata wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi. Wagombea hao Prof Phillemo Sarungi wa jimbo la Rorya na Christopher Kangoye wa Tarime, walifikwa na mkasa huo jana walipokuwa wakijinadi kwa wanaCCM. Sarungi na Kangoye waliuzwa maswali tofauti lakini walikwepa kijibu. Wakati profesa Sarungi akitakiwa kuwaachia vijana kinyang'anyiro hicho, Kangoye alitakiwa kueleza sababu za kung'ang'ania ubunge wakati aliwakuwa mkuu wa wilaya. Wananchi waliwataka waliwafanyia nini walipokuwa viongozi na sasa wanapanga kufanya nini ambacho wanadhani wengine watashindwa. Kangoye ambaye aliwahi kugombea ubunge katika jimbo hilo na kushindwa mara tatu alitwangwa maswali hayo katika kata za Manga, Komaswa na Nyandoto. Vijana hao walimtaka profesa Sarungi awaachia vijana ubunge kwa kuwa umri wake umepita. Huko Bunda, vurugu na vitisho vilitawala kwenye kampeni za kura za maoni katika jimbo la Bunda ambako wapambe wa baadhi ya wagombea walitishia kumwaga damu. Wagombea wanne juzi walitimua mbio katika kituo cha Manyamanyama na kumwacha Steven Wasira akijinadi peke yake. Wagombea hao walitimua mbio baada ya kundi la vijana linalodaiwa kuwa wapambe wa Wasira kuwafanyia fujo kwa kuwatukana na kuwarushia chupa. Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Elias Majura alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa wagombea hao wameandika barua ya malalamiko kwenda CCM na kupangiwa siku nyingine kufanya kampeni eneo hilo. Jimbo la Bunda linawagombea watano wa ubunge kutoka CCM ambao ni Yeremia Maganja, Ginche Kisase, Jeremiah John Wambura, Steven Wasira, Tumaini Mgaya na Emanuel John Charles Mkoa wa Mbeya SAKATA la wagombea ubunge kugoma kufanya kampeni Jimbo la Kyela limeingia katika sura mpya baada ya wagombea kuwakataa katibu wa CCM wilaya ya Kyela, Lwidiko Nong’onna na msaidizi wake Epmark Makuya kusimamia kampeni hizo. Habari zimeeleza kuwa wagombea hao hawataki viongozi hao kusimamia kampeni hizo kwa kuwa wanatuhumiwa kugawa kadi bandia. Juzi wagombea wanne waligoma kuanza kampeni wakidai kuwa na hofu ya kuhujumiwa kutokana na kuwepo kwa kadi walizodai kuwa zilizogawiwa kinyme na taratibu na viongozi hao. Nong’onna na msaidizi wake walishirikiana na mmoja wa wagombea hao kugawa kadi hizo kinyume cha taratibu ili kumsaidia katika kura za maoni. Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Verena Shumbusho zimeeleza kuwa wagombea hao waliwakataa katibu na msaidizi wake katika kikao kilichofanyika ofisi za CCM wilaya ya Kyela. Imedaiwa kuwa kadi za CCM zaidi ya 2,800 zimegawiwa katika Kata za Ikolo, Ikomba na Matema kinyume cha taratibu Mkoa wa Kigoma Wgombea nafasi za udiwani na ungue wilayani Kibondo, Kigoma wameipongeza kwa hatua yake ya kupambana rushwa katika kinyang’anyiro hicho. Thomas Buhahate ambaye ni mmoja wa wagombea katika jimbo la Muhambwe ,wilayani Kibondo alisema hatua hiyo itasadia kupata viongozi bora. Mkoa wa Arusha Kampeni za kuwania kuteuliwa kugombea ubunge zilianza kwa vituko katika majimbo ya Arusha mjini na Arumeru Magharibi, huku baadhi ya wagombea wakibanwa na maswali na kupokelewa kwa mabango. Katika kampeni hizo, ambazo wagombea wote wamekuwa wakiomba kuchaguliwa, viongozi wa CCM wa wilaya za Arusha na Arumeru mara kadhaa walijikuta wakiwatetea wagombea hasa wanaotetea nafasi zao kutokana na kubanwa zaidi na wananchi. Katika mkutano huo, Kileo aliwataka wanaCCM kuacha kupiga makofi wagombea wanapozungumza na hata kuwazomea, lakini hata hivyo, agizo hilo lilishindikana baada ya wananchi hao, kumpigia makofi mgombea Waziri wa nchi Ofisi ya makamu wa, Rais Dk Batilda Burian huku wakiguna alipoanza kuzungumza mbunge anayemaliza muda wake Felix Mrema. Mkoa wa Kilimanjaro TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro imewatia mbaroni wanachama watano wa CCM mjini Moshi akiwamo diwani mmoja wa chama hicho kwa kujihusisha na rushwa. Hata hivyo, mwanachama mmoja wa CCM ambaye ni mwanamke alifanikiwa kutoroka kupitia choo cha Wanawake wakati maofisa wa Takukuru wakisubiri afisa Mwanamke kufika eneo la tukio katika baa ya Peter Club Majengo. Bado haijawekwa wazi waliokamatwa walikuwa wakimkampenia Mbunge gani katika majimbo ya la Moshi Mjini na Jimbo la Moshi Vijijini ambayo ni majimbo yenye kashkashi nyingi za kampeni za mchakato ndani ya CCM. Kamanda wa Takukuru mkoani Kilimanjaro, Alexander Budigila aliwaambia waandishi wa habari jana jioni kuwa wanachama hao ambao ni mawakala wa mgombea mmoja wa ubunge, walitiwa mbaroni jana saa 8:00 mchana. Mkoa wa Ruvuma Wagombea nafasi ya ubunge kupitia CCM wa Jimbo la Peramiho wanaanza kampeni zao leo. Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa majimbo ya Songea Mjini, Mbinga Magharibi, Peramiho na Tunduru ndiyo yenye upinzani mkali kwa sasa. Mbinga Magharibi linawaniwa na Kapteni John Komba na Alex Shauri. Peramihoyupo Jennister Mhagama, na Joseph Mhagama na Jacob Mbawala. Songea Mjini ni Emmanuel Nchimbi, Oliver Mhaiki, Slim Slim, Renatus Mkinga na Said Nassor Moyo. Jimbo la Tunduru, mbunge wa sasa Mtutura Mtutura anachuana vikali na Msafiri Kandulinduli, Daimu Mpakate na Bakari Mkoa wa Iringa WANACHAMA wawili wa CCM waliokuwa wamechukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi ya udiwani katika kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa, wamejitoa baada ya kushindwa kulipa Sh 220,000 za uchaguzi. Wagombea waliojitoa katika kinyang’anyiro hicho ni Augustino Kimuliko na Bashil Mwamwindi ambao walidai kuwa hawakuataarifiwa mapema kama watatakiwa kulipa fedha. Wagombea hao walisema kuwa taarifa ya kuchangia fedha hiyo waliipata Julai 22 mwaka huu baada ya kurejesha fomu zao za kugombea katika kikao cha kamati ya siasa kilichofanyika katika ofisi za kata hivyo kuamua kujitoa. Katibu mwenezi wa CCM kata ya kihesa, Zainab Kufakunoga alikiri kujitoa kwa wanachama hao na kuongeza kuwa awali walijitoa wanne kati ya saba waliokuwa wamechukua fomu lakini walipopunguza kiwango cha fedha toka sh 220,000 hadi 150,000 wagombea wawili waliamua kurudi. Dar es Salaam VITUKO, ushirikina na madai ya kuzomeana vimetawala katika kampeni za ubunge kupitia CCM jimbo la Kigamboni. Wakiwa wamepanda kwenye basi moja kwenda vituo vya kujinadi, miongoni mwa wagombea 19 walipinga kutanguliwa na gari ya mmoja wao lililokuwa limebeba wapambe wake. Mmoja wa wagombea hao aliweka wazi kwamba, wamekwishakubaliana basi walilopanda lisitanguliwe na gari ya mgombea yeyote. Miongoni mwa wagombea hao walidai kwamba baadhi ya wapambe wa wagombea walikuwa wakifanya vitendo vya ushirikina ili wengine washindwe kujinadi mbele ya wanachama. "Dereva simamisha gari! Gari ile (iliyowatangulia) waelezwe waje nyuma na siyo mbele," alisema kwa hasira mmoja wa wagombea hao (jina tunalihifadhi). Waliokuwa wanadharau kuwa kuna ushirikiana, waliwaliwaza wenzao kwa kusema wasijali, wao wamwombe Mungu, kwa sababu ndiye mwenye nguvu zaidi kuliko nguvu za giza. Kituko kingine ni cha mbunge anayemaliza muda wake Abdulrahaman Mwichoum kulalamika kwamba mmoja wa wagombea ameandaa wapambe ili wamzomee. Katika jimbo la Ubungo, mmoja wa wasimamizi wa kampeni kuwataka wanachama wasiwaulize wagombea wa udiwani maswali magumu. Alidai kwamba kitendo hicho ni kuwapa mzigo wagombea hao ambao wote ni wa CCM bila sababu za msingi na kwamba maswali hayo magumu yahifadhiwe ili wawaulize wagombea wa vyama vya upinzani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu. “Sisi sote ni timu moja hivyo tukiulizana maswali magumu tunapoteza muda na kuwapa nafasi wapinzani. Ngojeni kura za maoni zikishapita ndipo mtauliza maswali yenu. Hawa ni wagombea wa CCM siyo wa upinzani,” alisema mmoja wa wasimamizi hao. Katika jimbo la Temeke mgombea mmoja alituma wajumbe kutoka kata nyingine kwa ajili ya kusiliza wagombea wenzake wanapojieleza na kuwarekodi. Hali hiyo ilijitokeza katika kata ya Chang’ombe ambako kundi hilo linalodaiwa kuletwa na mmoja wa wagombea hao kutoka Yombo Vituka, lilikuwa pia linagawa vitambulisho vya mgombea huyo. Habari imeandaliwa na Leon Bahati, Exuper Kachenje, Hussein Issa na Hidaya Kivatwa, Mkinga Mkinga na Jane Mapunda-Tudarco, Leon Bahati, Fredy Azzah, Zaina MalongoDar, Brandy Nelson, Mbeya, Mussa Juma na Hemedi Kivuyo, Arusha, Frederick Katulanda, Mwanza, Ibrahim Bakari, Songea, Hadija Jumanne, Samson Chacha na Antony Mayunga,Mara Mwisho www.mwananchi.co.tz |
0 comments:
Post a Comment