Malima alitaka haki itendeke
- CCM ikaweka ngumu
- Akaondolewa Wizara ya Elimu
WAZIRI wa Fedha Profesa Kighoma Malima, anazidi kuandamwa na baadhi ya vyombo vya habari, kutokana na rai yake kwa serikali ambayo alitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kupata ufumbuzi wa tatizo la wanafunzi Waislamu kubaki nyuma.
Hivi karibuni gazeti la Family Mirror limechapisha barua ambayo Profesa Malima alimwandikia Rais wa Jamhuri, wakati huo akiwa Waziri wa Elimu na kuinakilisha kwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, akipendekeza uchunguzi ufanyike ili kutatua tatizo hilo, lakini kwa makusudi ushauri huo umepotoshwa na gazeti hilo kuwa zilikuwa ni hila za siri za mwansiasa huyo kutaka kuwapa nguvu Waislamu.
Ukweli wenyewe ni huu kuwa, Profesa Malima hakulifanya jambo hilo kwa siri, na aliandika dokezo kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutumika hila katika kuwakwamisha wanawake na vijana wa Kiislamu kupata elimu ya juu, kwani kila wanapozidi kwenda mbele hesabu yao inazidi kupungua na akapendekeza iundwe tume kuchunguza tatizo hilo. Jambo hili ni uthibitisho wa dhahiri kuwa Profesa Malima alikuwa akitaka haki itendeke.
"Sio rahisi kupata maelezo yanayoeleweka ikiwa vijana hao katika shule za msingi wapo karibu nusu kwa nusu, baina ya Waislamu na wale wa madhehebu mengine, lakini inapofika sekondari, vyuo na vyuo vikuu idadi hiyo inapungua na kufikia asilimia 10-20", aliandika Profesa Malima katika dokezo lake kwa Rais.
Profesa Malima aliitahadharisha serikali dhidi ya kupuuza ushauri wake juu ya tatizo hili ambalo aliliita ni "nyeti", kuwa limeanza kuzungumzwa na vyombo vya habari vya nje kwa namna ya uchochezi, na akapendekeza tatizo hili litatuliwe kimya kimya kwa mpango wa muda mfupi na mrefu.
"Kwa maoni yangu", alizidi kuonesha njia Profesa Malima "tunaweza kufanya mambo mawili; tunaweza tukapuuza kwamba hakuna tatizo (wishing away the problem) wakati tatizo lipo dhahiri. Kufanya hivyo ni kuliahirisha kwani siku moja huko mbele ya safari litajitokeza na watu watataka kujua kwa nini", alifafanua na kuongeza; "pili tunaweza internally na hasa, kimya kimya tutalishughulikia".
Hata hivyo, gazeti la Family Mirror limeshindwa kueleza ukweli kuwa Rais Mwinyi alikubaliana na wazo hilo la Profesa Malima kuwa tatizo hilo lipo, lakini kutokana na unyeti wake akashauri lianze kuzungumzwa kwanza katika vikao vya Chama ili kama litakubaliwa, serikali ipewe agizo la kutekeleza kutoka kwenye chama.
Katika kujibu dokezo la Waziri Malima, Rais Ali Hassan Mwinyi kupitia Katibu wake alisema, "nionavyo mimi jambo hili ni nyeti na kwa ajili hiyo ni jepesi sana kufahamika vibaya na kuzusha mgogoro miongoni mwa wananchi, kwa vyovyote vile rai nyeti kama hii ingefaa kuanzia katika chama", alifafanua Rais.
Rais Mwinyi alizidi kuongeza kuwa, azimio la Musoma lililowapa upendeleo maalum wanawake lilianzia kwenye chama, na kwa sababu hiyo, Rais alimzuia Profesa Malima asiunde Tume juu ya jambo hili, lakini akamshauri abadilishane mawazo na Bi Mongela ambaye wakati huo alikuwa kama Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM.
Baada ya mawasilano hayo kilichofuatia ilikuwa ni vita maalum alivyopigwa Profesa Malima na barua yake hiyo iliibiwa na kutawanywa sehemu mbalimbali na hata baadhi ya viongozi fulani wa kidini walitaka Waziri huyo afukuzwe kazi, lakini hapakuwepo kigezo ambacho kingetumika na isieleweke vibaya.
Siku chache baadaye mtu mmoja ambaye jina lake hakupenda litajwe, na ambaye alikuwa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alilalamika katika gazeti la The Africa akidai serikali ya awamu ya pili ilipangwa kwa misingi ya kidini, na hivyo basi akapata fursa ya kuwataja Mawaziri wote Waislamu akiwemo Profesa Malima anatazamwa sana kama mtu ambaye mwenye msimamo wenye makosa kuwaelekea Waislamu.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichopendekezwa na Rais Mwinyi kutoa maelekezo juu ya kuondoa dhulma hii wakati huo kikiwa chini ya Uenyekiti wa Mwalimu, kimekaa kimya kuonesha jinsi wanamuhanga wa taifa hili wanavyokandamizwa makusudi katika medani hii muhimu ya elimu.
Pamoja na ahadi ya serikali, ilivyowekwa na Rais Mstaafu Mwalimu Nyerere mwenyewe ya kuweka uwiano katika elimu baina ya Waislamu na Wakristo kutotekelezwa, sasa ni wakati ambao rai ya Profesa Malima inajitokeza pale alipoonya kuwa jambo hilo lisipotatuliwa "ipo siku moja huko mbele ya safari likajitokeza na watu watataka kujua kwanini?"
Haki, Mei 10, 1995
MAKAMU Mwenyekiti wa CUF, Seif Shariff Hamad ambaye ametangaza nia ya kutaka kugombea Urais wa Zanzibar amewaeleza wananchi wa Matemwe kuwa CCM sasa hivi ni 'dhofulhali'.
Katika hotuba yake ambayo ilikuwa kali amesema, serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni ya kidhalimu na inavunja haki za binadamu.
Amesema, Shirika la kutetea haki za binadamu (Amnesty International) katika ripoti yake hivi karibuni ilieleza kuwa serikali ya Zanzibar ni ya kidikteta.
Akiufafanua udikteta huo, Seif alitoa mfano wa mkutano wa wanasheria wa Zanzibar ambao walitaka kufanya semina ili kujadili hali ya katiba. Mkutano huo, amesema, ulizuiwa na serikai ya Mapinduzi na pia semina hiyo haikufanyika.
Huku akishangiliwa na umati wa watu wa Matemwe Seif aliuliza, "hivi kuwazuia watu wasitoe maoni yao kuhusiana na mambo ya nchi yao ni halali? Je, hu si udhalimu? Huku si kuvunja katiba ambayo imewapa wanachi haki hiyo?
Jambo hilo, ameongeza kusema, limefanywa ili kuwazuia wanasheria wasitoe maon yao kuhusiana na mabadiliko ya 11 ya katiba ya Zanzibar ambayo inamtaka mtu awe ameishi mahali miaka mitano ndipo apate ruhusa ya kupiga kura.
Seif, amesema, pia kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuwamaliza "Wapemba". Huku akishangaa Seif aliuliza tena, "hivi hawa Wapemba humu Zanzibar ni adui?"
Akizungumzia matamshi ya Samwel Sitta alipokaririwa akidai kwamba yupo kiongozi mmoja wa CUF anataka kuvunja muungano, Seif Shariff alisema, "wewe Sitta hebu mtaje mtu huyo ni nani? Kwanini unasema kwa mafumbo?
Akizidi kuonesha kumshangaa Sitta, Seif Shariff alisema kuwa Waziri Sitta alisema kuwa lengo la mabadiliko ya 12 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ni kuwazuia Waarabu wasiichukue Zanzibar.
Huku akionesha kukasirika Seif alisema, "hivi Waziri mzima anaweza kusimama kwenye Bunge kutangaza ukabila? Hivi leo Tanzania ambayo ilikuwa na sifa ya kupiga vita ukabila duniani, imebadilika na kufuata sera za ukabila? Hivi Makaburu wa Kitanzania tayari wamezuka?
Akizungumzia muungano Seif amesema, wao wanayatambua mambo mawili tu ya muungano ambayo Karume na Nyerere walikubaliana mengine yote hawayatambui.
Amesema kuwa CUF itakapochukua nchi Zanzibar, basi yale mambo 12 yaliyoongezwa yeye atayafutilia mbali.
Aidha, amesema kuwa haki haiombwi bali haki huchukuliwa na ndivyo CUF itakavyofanya ikishinda uchaguzi hapo Oktoba 22.
0 comments:
Post a Comment