Chifu Masanja katoka Tanu kaingia Congress
CHIFU Francis Masanja wa Bukwimba na pia mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, nchini Tanganyika alitangaza jana kwamba amejiuzulu katika TANU na kuingia chama cha Congress.
Chifu Masanja ambae aliingia katika Baraza la Kutunga Sheria kwa tikiti ya TANU, amesema kwamba amechukua hatua hii baada ya kuona kile alichokiita mengine ya TANU sio ya faida kwa watu wa Tanganyika.
Katika taarifa yake magazetini Masanja anasema: Sasa nimeingia Congress, nami nitatoa siasa yake katika Baraza la Kutunga Sheria kwa sababu nimeshawishiwa kabisa kwamba ndio chama cha pekee ambacho bila woga au upendeleo, kinachunga haki za binadamu na kutoa maoni ya kweli ya watu wa nchi hii.
Sio Demokrasia
Alisema pia kwamba mara nyingi alisikia malalamiko kutoka kwa wanachama wa Wilaya yake na nyingine juu ya mambo yasiyo ya kidemokrasia yanayoendeshwa na wakuu wengine wa TANU.
"Kuna mambo mengine ambayo wakuu wa TANU waliwasumbua baba kabwela, bila ya kujali haki zao", alisema.
Chifu Masanja pia anasema kwamba TANU, kwa kutaka kura za watu, ilitoa ahadi nyingi kwa watu katika uchaguzi uliopita, lakini imeshndwa kabisa kutimiza ahadi hizo. Akasema wapiga kura hawaridhiki.
Hakuna Uhuru
Taarifa hiyo pia imesema kwamba ikiwa hali hii itaendelea nchi itachafuka na hakutakuwa na uhuru, na hasa uhuru wa kusema.
Alipoulizwa na mwandishi wetu kama amejiuzulu kwa sababu Uchifu umeondolewa, Masanja akajibu kwamba hiyo sivyo, na pia kwamba hana cheo chochote katika Congress bali ni mwanachama wa kawaida tu.
Msemaji wa TANU alipoulizwa kutoa maoni yoyote alisema kuwa hakuwa na maoni.
BAADA ya bendera ya Congress kutundikwa katika ofisi yao mpya huko Tanga, asubuhi mti wa bendera hiyo ukaonekana umekatwa na kuangushwa chini.
Hivi majuzi mjini Tanga ilifanyika sherehe ndogo ya kufungua ofisi kuu ya Jimbo ya chama cha African National Congress mtaa wa Ngamiani, barabara ya 15.
Katika sherehe hiyo, bendera nyekundu yenye alama nyeusi ya ‘T’ katikati ilitundikwa kama kawaida nje ya ofisi.
Baada ya kupepea kwa kutwa moja siku ya pili ikaonekana kwamba mti wa bendera umekatwa na kuangushwa chini.
Wakuu wa ofisi bado hawajatoa tamshi lolote na wala haijulikani kitendo hicho kimefanywa na nani, lakini polisi imearifiwa nayo inafanya uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment